Wednesday, December 26, 2012

0

UGONJWA WA KIFUA KIKUU NA DALILI ZA KIFUA KIKUU

Kifua kikuu ni ugongwa unaosababishwa na vimelea vidogo vidogo aina ya bakteria viitwavyo Microbacteria tuberculosis. Ugonjwa wa kifua kikuu unaenezwa kwa njia ya hewa kutoka katika mtu ambaye anaugua na hajaanza matibabu, mtu huyu akipiga chafya, kukohoa au kutema makohozi ovyo anaweza kuambukiza watu wengine.
Kifua kikuu kwa kawaida kinaathiri mapafu, pia kinaweza kuathiri sehemu yeyote ile nyingine ya mwili ikiwemo mifupa, tumbo na mgongo.
Dalili za kifua kikuu ni pamoja na kukohoa kwa wiki mbili au zaidi mfululizo, homa za mara kwa mara kwa wiki mbili au zaidi, kutokwa na jasho jingi hasa nyakati za usiku, kukohoa makohozi yenye damu, kupungua uzito zaidi ya kilo 3 ndani ya wiki 4 au kukonda pamoja na kukosa hamu ya kula.
Kifua kikuu hugundulika kwa kupima makohozi na ikibidi x-ray na matibabu yake ni bure katika hospitali zote za serikali na binafsi. Unapoona mtu ana dalili mojawapo kati ya hizi au wewe mwenyewe mshauri awahi kituo cha huduma za afya kwa uchunguzi na tiba au awasiliane na mratibu wa kifua kikuu na ukoma aliye karibu nae kwani mtu mmoja huweza kuwaambukiza watu kati ya 10 hadi 15 kwa mwaka kama hajapata matibabu. Wastani wa watu 176 huugua kifua kikuu kila siku nchini Tanzania na wastani wa watu 12 hufariki dunia kila siku .
Ikitokea umegundulika kuwa una kifua kikuu usihofu kwani kinatibika na mamilioni ya watu duniani kote wameugua na kupona. Unachotakiwa kufanya ni kufatisha masharti utakayopewa na daktari kama; kunywa dawa kila siku kwa muda uliopangiwa ili kupona kabisa. Matibabu yake huchukua kati ya miezi sita hadi minane.
Endapo umegundulika kuwa na kifua kikuu kumbuka kufunika mdomo na pua unapo kohoa au kupiga chafya, ili usiambukize watu wengine na pia usiteme mate ovyo.
Pumzika kiasi cha kutosha, kula chakula bora na uwafahamishe ndugu na marafiki kwamba unaugua kifua kikuu na uko kwenye matibabu, na ukisha kamilisha matibabu nenda kwa mhudumu wa afya kwa uchunguzi ili kuthibitisha kama umepona.
Kumbuka ni muhimu kuendelea kutumia dawa mpaka mwisho hata kama unajisikia vizuri ili usipate kifua kikuu sugu ambacho matibabu yake ni magumu. Mara wa mara kifua kikuu kimekuwa kikihusishwa na ugonjwa wa ukimwi kwani asilimia 50 ya watu wenye kifua kikuu wana VVU. Kama umethibitika una kifua kikuu ni muhimu kupata ushauri nasaha na kupima virusi vya UKIMWI, kwani asilimia 10-15 ya watu wanaoishi na VVU wanaugua kifua kikuu, hivyo ni muhimu kuchunguzwa kama una kifua kikuu ili kuboresha na kuokoa maisha yako kwani kifua kikuu kinatibika kabisa hata kama una maambukizi ya VVU.

0 comments: