Tuesday, January 22, 2013

0

MADHARA KWA MAMA MJAMZITO ATUMIAYE POMBE




              Baadhi ya wataalam wanasema unywaji wa wastani wakati wa ujauzito ni kitu ambacho kinaweza kukubalika ingawa wapo baadhi ya wataalamu wengine wanaoamini kuwa unywaji wa hata glasi moja ya mvinyo (wine) kwa wiki huhatarisha afya ya mtoto wako. Hata hivyo haijulikani kwa hakika, ni kiasi gani cha pombe ni salama kwa makuzi sahihi ya mtoto wako tumboni.
Wataalamu wengi wanashauri kuacha pombe kabisa wakati wa ujauzito. Pombe inaweza kuleta madhara makubwa kwa mtoto wako bila wewe kuhisi madhara yake. Na yanaweza kuwa madhara ya kudumu ambayo ataishi nayo maisha yake yote. Aidha kuna dhana imejengeka kwa baadhi ya wajawazito kuwa, hawatakiwi kunywa pombe kali kama vodka au whisky tu lakini ni ruksa kutumia aina nyingine za pombe. Hata hivyo dhana hii si sahihi kwa kuwa pombe za aina zote zaweza kuleta madhara makubwa kwa kiumbe aliye tumboni.
Kisayansi takwimu zinaonyesha kwamba unywaji sana wa pombe wakati wa ujauzito huathiri mimba. Ni hili hutokea zaidi katika kipindi cha miezi 3 ya mwanzo (first trimester), kipindi ambacho viungo vingi vya mwili wa mtoto hufanyika (organogenesis).
Nini hutokea unapokunywa pombe wakati wa Ujauzito?
Pombe ni sumu kwa mtoto. Unapokunywa pombe inaingia moja kwa moja kwenye mzunguko wa damu wa mama kasha hufika kwa mtoto kwa kupitia kondo la nyuma (placenta).
Mara pombe inapoingia kwenye mzunguko wa damu wa mtoto, huathiri uwezo wa mtoto kupata chakula, virutubisho na oksijeni ya kutosha kwa ajili ya maendeleo ya kawaida katika ubongo na viungo vingine. Hii inaweza kuathiri ubongo wa mtoto na ukuwaji wa viungo vya mwili kwa ujumla. Uharibifu huu unaweza kuathiri uwezo wa mtoto kujifunza na kufikiri pindi anapozaliwa hali ambayo itajionesha kwa matendo yake kama mtoto na kama mtu mzima.
Aidha, utafiti umeonesha kwamba uwezo wa mimba kustahimili kiwango cha pombe ni mdogo mno hali ambayop huathiri ufanyikaji wa viungo na ukuwaji wake kwa kiasi kikubwa.
Kwa kiasi gani mtoto wako ambaye hajazaliwa anaweza kuathiriwa na pombe?
Kiwango cha kuathirika kwa mimba kutokana na unywaji pombe unaofanywa na mama mjamzito hutegemea sana mambo makuu matatu ambayo ni:
  • Kiasi cha unywaji wa pombe
  • hatua ya mimba yaani umri wa mimba
  • mara ngapi unakunywa pombe
Matatizo yatokanayo na unywaji wa pombe
Baadhi ya madhara yanayoweza kumpata kiumbe aliye tumboni kwa mama kutokana na unywaji wa pombe kipindi cha ujauzito ni pamoja na
  • Kutoka/kuharibika kwa mimba
  • Mtoto kuzaliwa akiwa na uzito mdogo
  • Mtoto kuzaliwa akiwa na ulemavu wa mbavu na kidari (sternum)
  • Mtoto kuzaliwa akiwa na matatizo ya mgongo uliopinda (kibiongo) na vidole vilivyoundana
  • Mtoto kuzaliwa akiwa na kichwa kidogo kuliko kawaida (microcephaly)
  • Mtoto kuzaliwa akiwa na matatizo ya pua
  • Kuzaliwa na matatizo ya taya
  • Mtoto kuwa na matatizo ya kutokuona mbali
  • Matatizo ya moyo kama vile moyo kuwa na tundu
  • Matatizo ya figo
  • Mtoto kuwa na ubongo mdogo na pia matatizo ya akili
  • Mtoto kuzaliwa akiwa na mdomo sungura (lip palate na cleft palate)
  • Matatizo ya kimaumbile ya masikio na ulemavu kwenye sehemu za uzazi (genital malformations).
  • Aina mojawapo ya kansa ya chembe nyeupe za damu (Acute Myeloid Leukemia). Hii ni kwa mujibu wa utafiti uliochapishwa katika jarida moja la utafiti wa kansa la Marekani lijulikanalo kama Journal of the American Association for Cancer Research.
Ieleweke kuwa, madhara haya si ya muda bali ya kudumu ambayo yanaweza kusababisha kifo kwa mtoto, malezi na makuzi ya tabu na hata hisia mbalimbali katika maisha.
Kama wewe ni mjamzito, ni vizuri kuacha kunywa pombe. Hata hivyo wanawake ambao walikuwa wanatumia pombe wakati wa ujauzito wasiwe na hofu sana na habari hii. Kuna msemo uliozoeleka kitabibu kuwa ‘si kila mvutaji wa sigara anapata kansa ingawa ukweli ni kuwa wavutaji wapo katika hatari kubwa zaidi’. Hali hii pia ina ukweli linapokuja suala la unywaji wa pombe wakati wa ujauzito kwamba si kila mtoto anaathiriwa na unywaji wa pombe ingawa hatari ya kuathirika ni kubwa zaidi. Hivyo basi ni muhimu kwa mama mjamzito kufanya maamuzi sahihi ya maisha ya mtoto wake.

0 comments: