Saturday, October 13, 2012

3

HISTORIA FUPI YA MWALIMU NYERERE MPAKA MAUTI YALIPOMFIKA

Tarehe ya kuzaliwa 13 Aprili 1922
Mahali pa kuzaliwa Butiama
Tarehe ya kifo 14 Oktoba 1999
Rais wa Tanzania
Alingia ofisini 1964
Aliondoka ofisini 1985
Alitanguliwa na (alikuwa rais wa kwanza)
Alifuatwa na Ali Hassan Mwinyi
Dini Mkristo Mkatoliki
Elimu yake Chuo Kikuu cha Edinburgh - Uskoti Digrii anazoshika M.A. ya historia na uchumi
Kazi mwalimu, mwanasiasa Mengine Nyerere alikuwa mwenyekiti wa chama cha TANU na baadaye wa CCM.

Mara nyingi aliitwa "Mwalimu Nyerere".

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikuwa rais wa kwanza wa Tanzania. Alizaliwa Butiama, mkoani Mara pembezoni mwa Ziwa Nyanza tarehe 13 Aprili, 1922. Alifariki dunia 14 Oktoba, 1999. Aliiongoza Tanzania toka mwaka 1961 hadi mwaka 1985.

Yeye ni mwasisi wa itikadi ya ujamaa na kujitegemea. Kabla ya kuingia kwenye siasa alikuwa ni mwalimu. Kazi hii ndiyo ilimpatia jina ambalo lilimkaa maisha yake yote la "Mwalimu." Mwalimu Nyerere ni kati ya viongozi wachache wa Afrika ambao wameacha madaraka kwa hiyari baada ya kutawala kwa muda mrefu. Alipostaafu urais mwaka 1985 alirudi kijijini kwake Butiama ambako aliendesha shughuli za kilimo. Aliendelea kuwa na athari kubwa katika siasa ya Tanzania hadi kifo chake.

Maisha Ya Mwalimu

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alizaliwa mwaka 1922 ( katika kijiji cha Butiama, wilaya ya Musoma, mkoa wa Mara, Tanzania (wakati ule: Tanganyika). Alikuwa mojawapo kati watoto 26 wa Nyerere Burito, chifu wa kabila la Wazanaki. Alipokuwa mtoto Nyerere alichunga mifugo ya babake; katika umri wa miaka 12 aliingia shule akitembea kilomita 30 hadi Musoma. Baada ya kumaliza shule ya msingi aliendelea kusoma shule ya wamisionari Wakatoliki huko Tabora. Katika umri wa miaka 20 alibatizwa akawa mkristo Mkatoliki hadi mwisho wa maisha yake.

Mapadre wakaona akili yake wakamsaidia kusoma ualimu huko Makerere, Kampala, Uganda kuanzia 1943 - 1945. Makerere akaanzisha tawi la Umoja wa wanafunzi Watanganyika pia amejihusisha na tawi la Tanganyika African Association (TAA). Baada ya kumaliza masomo ya ualimu alirudi Tabora akifundisha shule ya St.Mary´s. Mwaka 1949 alipata skolashipu ya kwenda kusoma kwenye Chuo Kikuu cha Edinburgh huko Uskoti /Uingereza akasoma M.A. ya historia na uchumi(alikuwa mtanzania wa kwanza kusoma katika chuo kikuu cha Uingereza na mtanzania wa pili kupata shahada ya elimu ya juu nje ya Tanzania).

Aliporejea Tanganyika kutoka masomoni, Nyerere alifundisha Historia, Kingereza na Kiswahili katika shule ya St. Francis iliyo karibu na Dar es Salaam. Mwaka 1953 alichaguliwa kuwa raisi wa chama cha Tanganyika African Association (TAA), chama ambacho alikisaidia kukijenga alipokuwa mwanafunzi katika chuo kikuu cha Makerere. Mwaka 1954 alikibadilisha chama cha TAA kwenda katika chama cha Tanganyika African National Union (TANU) ambacho kilikuwa cha kisiasa zaidi kuliko TAA. Ndani ya mwaka mmoja chama cha TANU kilikuwa tayari chama cha siasa kinachoongoza Tanganyika.

Uwezo wa mwl. Nyerere uliwashitua uongozi wa kikoloni na kumlazimisha Nyerere kuchagua kati ya siasa na kazi ya ualimu. Nyerere alisikika akisema kuwa alikuwa mwalimu kwa kuchagua na mwanasiasa kwa bahati mbaya. Alijiuzuru ualimu na kuzunguka nchini Tanganyika kuzungumza na watu wa kawaida na machifu ili kuleta muungano katika mapigano ya uhuru. Pia alizungumza kwa niaba ya TANU katika Trusteeship council na Fourth committee ya Umoja wa Mataifa (UN) huko New York. Uwezo wake wa kimaongezi na kuunganisha watu ulimwezesha kufanikisha Tanganyika kupata uhuru bila umwagaji wa damu. Ushirikiano mzuri aliouonyesha aliyekuwa gavana wa wakati huo bwana Richard Turnbull ulisaidia pia kuharakisha upatikanaji wa uhuru. Nyerere aliingia katika bunge la kikoloni mwaka 1958 na kuchaguliwa kuwa waziri mkuu mwaka 1960. Mwaka 1961 Tanganyika ilipata uhuru wake na tarehe 9/12/1961 Nyerere alichaguliwa kuwa waziri mkuu wa Tanganyika huru na mwaka mmoja baadae Nyerere alikuwa raisi wa kwanza wa jamhuri ya Tanganyika. Nyerere alikuwa kiungo muhimu katika muungano wa Tanganyika na Zanzibar kutengeneza Tanzania baada ya mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964 yaliyomtoa madarakani sultani wa Zanzibar Jamshid bin Abdullah.

Sifa zake

Bado anakumbukwa na watanzania hasa wa hali ya chini kutokana na sera zake za kujali utu na ubinadamu.Pia ataendelea kukumbukwa na waafrika kote barani hasa kwa mchango wake mkubwa wakati wa harakati za kupigania uhuru katika nchi mbali mbali barani Afrika.

Ni mmoja wa viongozi wachache wanaokumbukwa kwa kutojilimbikizia mali pamoja na kutawala kwa miaka zaidi ya 24.

Mwishoni mwa maisha yake Nyerere aliishi kama mkulima wa kawaida kijijini kwake Butiama. Alipatwa na kansa ya damu (leukemia) na kufariki Uingereza wakati wa kutibiwa katika mji wa London tarehe 14 Oktoba, 1999. Alizikwa mahali pa kuzaliwa kwake, kijiji cha Butiama.

Machapisho ya mwl.Julius K. Nyerere.

• Freedom and Socialism.Mkusanyiko wa maandiko na hotuba, 1965-1967 (1968)

• Freedom & Development, Uhuru Na Maendeleo (1974)

• Ujamaa - Essays on Socialism' (1977)

• Crusade for Liberation (1979)




3 comments:

  1. Nimekuelewa vzuri ila nna swali kumekuwa na maneno yanazungumzwa kwamba mwalimu alikiongoza chama cha mapinduI hadi mnamo mwaka 1990 toka 1977

    ReplyDelete
  2. Mwalimu Nyerere alizikwa tarehe ngapi

    ReplyDelete